MEYA KIBAHA AWAHIMIZA WAZAZI WA WANAFUNZI KUSHIRIKI UJENZI WA MIUNDOMBINU YA SHULE

Na Gustaphu Haule, Pwani
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dr. Mawazo Nicas amewataka wazazi wa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya shule ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Dr.Nicas ametoa kauli hiyo Septemba 17/2026 wakati akizungumza na Wazazi,walimu ,Wanafunzi na viongozi mbalimbali katika mahafali ya 17 ya Shule ya Sekondari Pangani iliyopo Kata ya Pangani Manispaa ya Kibaha.
Amesema kuwa wazazi hawana budi kushirikiana na Kamati za Shule katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya Shule ikiwemo ofisi za walimu na baadhi ya miundombinu mingine na badala yake waache kutegemea serikali wakati wote.
Dr.Nicas amesema,haiwezekani kuna kuwa na Shule kongwe ila walimu wake hawana sehemu za kukaa na kuishia kukaa kwenye vibaraza vya madarasa jambo ambalo sio zuri na halileti picha nzuri.
Amesema, kila mzazi akiamua kuchangia matofali matatu au manne, kwa wanafunzi wote waliopo basi ofisi za walimu zitajengwa na jambo hilo linaweza kufanyika kwa ushirikiano na Manispaa ikiona mmefikia hatua fulani itaunga mkono juhudi za wananchi au wazazi.
Amesema Serikali imeendelea kusisitiza elimu bure ila kuna michango ambayo wazazi huwa wanakubaliana kwenye vikao vya Kamati za shule kwa ajili ya kuchangia mambo mbalimbali ikiwemo mitihani lakini bado wapo Wazazi wanashindwa kutoa ila kwenye michango ya harusi anakuwa mstari wa mbele.
"Wapo wazazi hapa wakiambiwa hela ya mtihani Sh.1000 atasema hana ila kukata sare za vijora na michango ya harusi anakuwa mstari wa mbele kutoa na tuseme jambo hili sio zuri wazazi tushirikiane na walimu kujenga taaluma bora kwa vijana wetu hawa," amesema Dr.Nicas
Mkuu wa Shule ya Sekondari Pangani Tatu Mwambala,amesema mwaka 2025/2026 Shule yake imepata fedha za miradi ya maendeleo kutoka Manispaa ya Kibaha kiasi cha Sh.milioni 38 ambazo zilitumika kukarabati maabara ya somo la Chemia na kujenga matundu ya vyoo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali pamoja na wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Pangani.
Mwambala amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha miundombinu ya shule ili kutoa fursa kwa watoto wa Kitanzania kupata elimu.
Amesema pia, Shule yake ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya viti na meza lakini ameishukuru Manispaa ya Kibaha kupitia uongozi wa Mkurugenzi Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kutoa viti na meza vya wanafunzi 227 ambayo imeondoa changamoto ya wanafunzi kukosa sehemu ya kukaa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akiendesha harambee ya kula keki kwa ajili ya kuchangia fedha za ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari Pangani hafla ambayo ilifanyika Septemba 17/2026.
Mwambala,amesema kuwa pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Shule yake lakini bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa uzio wa Shule hali ambayo inapelekea wanafunzi kutoroka, usalama wa wanafunzi kuwa mdogo,huku nyingine ni ukosefu wa vyumba vya utawala, ukosefu wa mabweni na uchakavu wa miundombinu ya shule.
Mwambala amemuomba Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas kushirikiana na viongozi wengine,Wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha ujenzi wa uzio huo unafanikiwa kujengwa ili kuwapa wanafunzi mazingira mazuri ya kujisomea ikiwemo kulinda usalama wao.
Hata hivyo,Mwambala amesema kuwa Shule ya Sekondari Pangani inajumla ya wanafunzi 881 kati yao wanaume 335 na Wanawake 546 ambapo wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2026 ni 157 .
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akimuendesha mmoja wa wanafunzi mlemavu anayehitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Pangani .




Post a Comment